
 | | TODAY: | Tue, Feb 09, 2010 6:11pm EAT |  |
Kyanguli: Waalimu wafungwa jela miezi 8Written By:Lillian Mkabane , Posted: Tue, Jan 29, 2002
Mwalimu mkuu wa shule ya Mseto ya Kyanguli na naibu wake wamehukumiwa kifungo cha miezi minane gerezani kwa kukosa kuzuia moto ulioteketeza Bweni na kusababisha vifo vya wanafunzi 67 mwaka jana.
Mwalimu huyo mkuu David Mutiso Kiilu na naibu wake Stephen Kasyoka Makau walihukumiwa na hakimu mwandamizi wa Nairobi Rosemelle Mutoka baada ya kubainika kwamba wote walishindwa kuchukua hatua zifaazo kuzuia kuchomwa kwa bweni hilo licha ya kupashwa habari juu ya kuweko mpango kama huo.
Akipitisha hukumu hiyo, Bi. Mutoka alisema waalimu hao wawili walionyesha hali ya kutojali katika utekelezaji wa kazi yao na kukosa kuwalinda wanafunzi 100 waliokuaw chini ya ulinzi wao.
Alisema ingawa amezingatia hali ya masikitiko ya watuhumiwa hao kufuatia vifo vya wanafunzi wao sharti walimu wengine wakuu wapate funzo kutokana na hali ya kuongezeka kwa ghasia shuleni.
Alisema waalimu hao walikuwa wamepashwa habari kuhusu harufu ya mafuta ya petroli karibu na bweni lililoteketea mnamo tarehe 24 na tarehe 25 mwezi March mwaka uliopita lakini walifanya msako hapo kwa masaa 20 bila kujali kuendeleza msako wao hadi sehemu nyingine yakiwemo masanduku ya wanafunzi.
|
|  |