Bunge la kaunti ya Kwale limeidhinisha hoja ya kumng’atua afisini waziri wa masuala ya jamii na ukuzaji wa talanta kaunti hiyo Ramadhan Bungale.
Kiongozi wa wengi katika bunge hilo James Dawa amesema kuwa sasa hatma ya Bungale itaamuliwa na kamati maalum ya bunge hilo.
Dawa ambaye pia ni mwakilishi wa wadi ya Puma amesema waziri huyo atapewa nafasi ya kujitetea mbele ya kamati hiyo kufuatia madai ya ufujaji wa fedha za umma yanayomkabili.
Ni kauli iliyoungwa mkono na mwakilishi wa wadi ya Ramisi Raia Mkungu anayesema kuwa Bungale hafai kushikilia afisi yoyote ya serikali.
Kulingana na Mkungu, waziri huyo anakabiliwa na madai ya ubadhirifu wa fedha ya shilingi milioni 65 zilizotolewa kama mkopo kwa wafanyibiashara mwaka wa 2017.
PICHA KWA HISANI