Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt. Fred Matiang’i ametoa changamoto kwa wahasibu wote nchini kujitokeza na kushirikiana na mashirika mengine ya kiserikali katika vita dhidi ya ufisadi.
Matiang’i amewahakikishia wataalamu hao kwamba sheria itawalinda dhidi ya waajiri na wateja ambao watalipiza kisasi katika kesi ambapo watafichuliwa kwa ufisadi.
Akizungumza wakati wa kongamano la 39 ya kila mwaka kuhusu Taasisi ya Wahasibu Walioidhinishwa wa Uhasibu wa Umma nchini ICPAK, Matiang’i amewapa wahasibu jukumu la kuhakikisha kwamba rasilimali zinazotengewa afisi za umma zinalindwa na kuhifadhiwa kwa kuhakikisha shughuli zozote zinazofanywa zimeandikwa ipasavyo.
Matiang’i pia aliibua wasiwasi kufuatia ongezeko la visa vya ufisadi vilivyorekodiwa katika tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) zikiwemo zile zinazohusisha wahasibu walioiomba ICPAK kuwaadhibu wanachama wao wanaohusishwa na ufisadi.
Alisema katika matukio kadhaa, wahasibu wameshindwa kuripoti au kusajili vitendo vya udanganyifu vinavyotokea katika sekta za umma na kukosa umakini katika matumizi ya Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Fedha (IFMIS) unaosababisha ubadhirifu wa fedha za umma.
Kulingana na Utafiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Ulaghai wa mwaka 2020, kampuni za humu nchini zimeripotiwa kupoteza Shillingi billion 5.5 kutokana na ufisadi.
Hata hivyo waziri huyo amesema kuwa zaidi ya asilimia 14 ya hasara ya Shillingi bilioni 5.5 ilitokana na udanganyifu wa taarifa za uhasibu na fedha.