Familia mbili zinazoishi katika eneo la Bamburi eneo bunge la Kisauni wanaiomba serikali iingilie kati iwasaidie kuwatafuta vijana watatu miongoni mwao ni wana wao wawili ambao wanadai walipotea tangu juma lililopita.
Wakiongozwa na mamake mmoja wa vijana hao waliopotea Zahra Omar wanaeleza kuwa watoto wao hawahusiki na visa vyovyote vya kihalifu na wanashangaa ni kwanini hadi kufikia sasa hawajapata kuwaona watoto wao.
Kwa mujibu wa Bi. Omar, Hussein Mohammed na Fahmi Bakari watoto hao wako na hulka njema na wanajishughulisha na kazi katika sekta ya Matatu.
Kwa upande wake mkewe Hussein Mohammed,Bi. Asli Isack anadai kuwa mume wake alikuwa amesafiri kwa shughuli za biashara za ununuzi wa matatu akiwa na wenzake na kuitaka serikali iwasaidie kupata wapendwa wao.
Hata hivyo afisa wa kushughulikia maswala ya dharura katika shirika la kutetea haki za kibinadamu la HAKI AFRIKA hapa Mombasa Alexander Mbela anasema kuwa takwimu walizofanya takriban vijana 63 wamekamatwa kwa njia tatanishi na akaeleza wameweka mikakati mbadala ya kushughulikia maswala hayo.