Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho amepinga madai kwamba uhusiano baina yake na Gavana wa Kilifi Amason Kingi umeanza kusambaratika kufuatia hatua ya kutaka kugombea kiti cha Urais kupitia tiketi ya Chama cha ODM.
Madai hayo ni ambayo yaliibuliwa baada ya Kingi kukosa kuhudhuria mkutano ulioongozwa na Gavana Joho katika Kaunti ya Lamu kufanikisha mpango wa eneo la Pwani kuungana.
Joho amesema kwamba Kingi siku hiyo alipaswa kukutana na Wawakilishi Wadi jinsi ilivyoafikiwa wakati wa mkutano uliowaleta pamoja magavana wanne wa Pwani katika Kaunti ya Tatita Taveta tarehe kumi mwezi huu.
Magavana hao alikuwa Joho, Kingi, yule waTaita Taveta Granton Samboja na wa Tana River Dhadho Godhana.
Kauli ya Joho imejiri kufuatia taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini kwamba Kingi amejitenga naye kufuatia hatua yake ya kutaka kuipeperusha bendera ya ODM katika kinyang’anyiro cha Urais mbali na ilivyodhaniwa kwamba angefanya hivyo kupitia Chama cha Pwani ambacho kilikuwa kianzishwe.
Joho hata hivyo ameshikilia msimamo wa kufanikisha azma kuipeperusha bendera ya ODM.