Naibu wa kamishna katika kaunti ndogo ya Ganze Evans Nyaberi amelitaka shirika la Kilifi Citizen Forum Kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi wa eneo hilo kwani imesaidia kuboresha uhusianao mwema baina ya wenyeji na viongozi.
Akizungumza na meza yetu ya habari katika eneo hilo Nyaberi ameelezea kuwa kwa miaka miwili sasa tangu shirika hilo kuanza shughuli hiyo wananchi wameonekana kuwa na uhusiano mwema na viongozi wao na hivyo kuwataka washikadau katika shirika hilo kutositisha zoezi hilo.
Hata hivyo, ametaja hatua ya baadhi ya wananchi kukosa kujua pahala pa kupeleka lalama zao kama mojawapo ya changamoto walizokumbana nazo hapo awali huku kamishna Tobias Sambu akisema kuwa hamasa zinazotolewa na shirika hilo zimewasaidia pakubwa katika kurahisisha utendakazi wao.
Aidha, Sambu amelitaka shirika hilo kuongeza idadi ya wawakilishi wa wananchi katika bunge hilo la mwananchi hasa wale walioko nyanjani ili kuweza kuwafika wote ikifahamika kuwa eneo hilo ni kubwa sana.