Naibu kamishena wa Kilifi eneo bunge la Rabai, Musa Salat, amewahakikishia wakaazi wa Rabai usalama taifa linapojiandaa kwa kipindi cha kampeni za kisiasa.
Kwa mujibu wa Salat, kufikia sasa hali iko shwari eneo hilo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya wadau wote kuhakikisha kuwa jamii inaishi kwa amani.
Afisa huyo wa utawala, aidha amedokeza kuwa ushirikiano mwema baina ya viongozi mbali mbali wa mashinani ndio imekuwa ngao ya umoja na utangamano.
Wakati huo huo, Salat ameonya wale wenye nia ya kuharibu amani wakati wa kampeni kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Kulingana na mwenyekiti huyo wa usalama Rabai, kila mwanasiasa yuko huru kufanya kampeni popote kwa kuzingatia kanuni za kiusalama na sheria za uchaguzi nchini.