Familia moja kutoka eneo la Kadzandani kwenye eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi inaiomba serikali pamoja na wahisani kujitokeza ili kumsaidia mtoto wao Philip Shukrani Maitha kujiunga na shule ya upili.
Kulingana na mamake mvulana huyo Bendera Maitha Mweni ambaye pia anaugua ugonjwa wa saratani ya mfuko wa kizazi, mtoto wake ameshindwa kujiunga na shule ya upili kutokana na upungufu wa kifedha.
Mweni aidha anasema licha ya changamoto kubwa ya kiafya anayoipitia, nia yake kuu ni mtoto wake kupata msaada wa kuendelea na masomo.
Kwa upande wake mvulana huyo Philip Shukran Maitha ambaye alipata alama 298 na kuitwa katika shule ya upili ya Ganze amewaomba wahisani kumsaidia kuendelea na masomo yake ili kutimiza ndoto zake.
Maitha anadai kuwa kwa sasa hana msaada wowote wa kujiunga na shule ya upili kutokana na maradhi anayopitia mamake, hali inayomlazimu kumhudumia kila wakati.