Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 hapa nchini kimepungua hadi asilimia 0.6, huku watu 20 zaidi wakibainishwa kuambukizwa ugonjwa huo kutoka kwa sampuli 3,444 zilizopimwa.
Idadi jumla ya visa vilivyobainishwa hapa nchini sasa imeongezeka hadi 253,833,huku zaidi ya sampuli millioni 2.7 zikiwa zimepimwa. Katika maambukizi ,kaunti ya Nairobi imeongoza kwa visa 8,Kajiado 3 na Uasin Gishu visa viwili.
Kaunti za Busia, Elgeyo Marakwet , Kakamega , Kiambu , Lamu, Murang’a na Nakuru zimenakili kisa kimoja kila moja .
Kwenye taarifa, waziri wa afya Mutahi Kagwe, alisema wagonjwa 57 wamepona,mmoja kutoka hospitalini ilhali 56 walikuwa wakiuguzwa nyumbani.Hata hivyo watu saba wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo ,na kuongeza idadi jumla ya vifo hadi 5,312.
