Matayarisho ya mazishi ya washirika 33 wa kwaya ya kanisa walioangamia siku ya Jumamosi wakati basi lao liliposombwa na maji katika mto Enziu katika kaunti ya Kitui yameanza.
Askofu wa kanisa katoliki katika kaunti ya Kitui Joseph Mwongela alisema kuwa miili ya wanakwaya wote waliokuwa katika basi hilo imeopolewa kutoka katika mto huo. Waziri wa afya katika serikali ya kaunti ya Kitui Winnie Kitetu amesema kuwa uchunguzi wa DNA utafanyiwa miili ya watoto na kuwa tayari kufikia siku ya Ijumaa.
Alisema kuwa miili ya watu wazima itatolewa kwa jamaa zao pindi tu baada ya kukamilika kwa kuchukuliwa kwa alama za vidole. Basi hilo la shule lililokuwa limewabeba wanakwaya wakielekea katika eneo la Nuu ili kuhudhuria sherehe ya harusi lilisombwa na maji likijaribu kuvuka mto Enziu siku ya Jumamosi.
Mabaki ya basi hilo yaliondolewa katika mto huo siku ya Jumapili usiku.