Mgombea ugavana wa chama cha Wiper kaunti ya Mombasa Mike Mbuvi Sonko ameahidi kuleta mabadiliko kupitia miradi ya maendeleo kwa wakaazi wa Mombasa.
Wakizungumza katika eneo bunge la Changamwe katika kaunti ya Mombasa baada ya ziara yao kutoka Machakos kwenye barabara kuu ya Mombasa road, kiongozi wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo, Sonko na mgombea mwenza Ali Mbogo waliwahakikishia wakaazi mabadiliko mara watakapochaguliwa kuingia afisini.
Sonko alikariri kuwa katika muda wa siku 100 za kwanza serikali yake itatenga fedha ambazo zitatumika kuwawezesha vijana na wanawake wasio na ajira katika kaunti ya Mombasa.
Sonko alibainisha kuwa serikali yake itashughulikia suala la ukosefu wa usalama katika kaunti hiyo ambalo limeendelea kushuhudiwa.
Kalonzo alisema kuwa Sonko anafaa kuwania kama gavana wa Mombasa ili kurejesha utukufu wake uliopotea.
Sonko baadaye alizuru kaburi la mamake kwenye makaburi ya kikowani hapa mjini Mombasa.