Naibu wa rais William Ruto amesema kuwa mfumo wake wa kiuchumi almaarufu Bottom-Up utasaidia pakubwa kuboresha maisha ya mamilioni ya wakenya.
Ruto ambaye alikuwa kwenye ziara katika kaunti ya Makueni, alisema kuwa mfumo huo wa kiuchumi utazindua muamko mpya ambao utaangazia kubuni mazingira mwafaka ya uwekezaji na kutoa kipau mbele kwa biashara ndogo ndogo.
Ruto anasema kuambatana na mfumo huo wa kiuchumi, kunawiri kwa biashara kutazalisha mapato na kubuni nafasi za ajira, hususan kwa vijana.
Naibu Rais alisema amejitolea sio tu kuwapa nguvu WaKenya wa kawaida katika ngazi za mashinani bali pia kuunganisha taifa hili.
Aliwataka wapinzani wake kushindana naye katika jukwaa la maswala ya maendeleo kwa vile hakuna nafasi tena kwa siasa za ukabila na migawanyiko katika taifa hili.