Wafuasi wa chama cha PAA katika eneo la rabai kisurutini kaunti ya Kilifi wamekitaka chama hicho kuandaa upya zoezi la kura za mchujo baada ya idadi kubwa ya wanachama wake kutoona majina yao kwenye sajili ya wapiga kura.
Akizungumza baada ya kushindwa kupiga kura katika kituo cha shule ya msingi ya kajiwe, mwaniaji kiti cha uwakilishi wadi ya Rabai Kisurutini, Saidi Charo Kaingu amestaajabishwa baada ya kuona jina lake limeandikwa visivyo na hivyo kushindwa kujipigia kura.
Baadhi ya wanachama waliojitokeza katika mchujo huo aidha wamelalamikia swala hilo hilo la kutopata majina yao katika sajili ya wapiga kura.
Hata hivyo baadhi wamepata majina yao na kuweza kuendeleza haki yao ya kikatiba.
Aidha afisa anayehusika na maswala ya uchaguzi katika chama cha PAA Edward Mwachinga, kupitia njia ya simu, amesema amepokea taarifa hiyo na kuahidi kuliangazia kwa kina suala hilo.