Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga anatarajiwa kubaini hatima yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao kwenye mkutano wa Azimio la Umoja katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.
Mkutano huo unatarajiwa kuwaleta pamoja wajumbe maalum waalikwa wanaokisiwa kuwa 10,250 kutoka maeneo mbalimbali humu nchini.
Zaidi ya magavana 30 kutoka maeneo mbalimbali nchini na maseneta zaidi ya 40 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.
Aidha wabunge zaidi ya 200 na zaidi ya waakilishi wa wodi 1,500 wanatarajiwa kuhudhuria.
Mbunge wa Suna mashariki Junet Mohamed alikuwa amesema awali kuwa uwanja huo utafurika huku akitarajia viwambo vya runinga kuwekwa nje ya uwanja huo kuwawezesha wale ambao hawataweza kuingia uwanjani kufuatilia matukio moja kwa moja.
Mashirika ya usalama pia yametoa hakikisho la kuwepo kwa usalama wa kutosha huku watakaohudhuria wametakiwa kuzingatia masharti yaliyowekwa kudhibiti kusambaa kwa janga la COVID-19.