Safaricom Golf Tour itaingia mkondo wake wa nane wikendi hii katika uwanja wa golf wa daraja la 71 wa Nyali katika Kaunti ya Mombasa.
Michuano ya Nyali inajiri wiki moja baada ya mkondo wa saba wa ziara hiyo iliyoandaliwa katika Klabu ya Karen Country wiki jana ambayo ilishuhudia Don Riaroh mwenye umri wa miaka 70 na Muriithi Gatu mwenye umri wa miaka 9 wakitaja washindi wa jumla katika mashindano ya makampuni na ya vijana mtawalia.
“Tunapoanza nusu ya pili ya ziara yetu ya kwanza ya gofu, tunasalia na matumaini juu ya athari inayopatikana. Tumewafikia takriban vijana 3,000 kupitia kliniki, mashindano ya vijana na programu za uhamasishaji na tunatazamia kutangamana na vijana zaidi kutoka Pwani wikendi hii”, amesema Peter Ndegwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Safaricom.
Mashindano ya wikendi pia yanaashiria Safaricom Golf Tour ya kwanza kufanyika katika eneo la pwani. Hafla hiyo imevutia wacheza gofu 220 wakuu na zaidi ya vijana 50, kutoka kaunti zote sita za Pwani zikiwemo Mombasa, Kilifi, Kwale, Lamu, Tana River na Taita Taveta.
Mashindano ya ushirika yamepangwa kufanyika Jumamosi huku vijana wakijifua kwenye kozi Jumapili kando na kliniki ya gofu katika kituo hicho.
Safaricom Golf Tour hadi sasa imepitia maeneo saba kote nchini ambayo ni: Nanyuki, Limuru, Muthaiga, Nyanza, Machakos, Eldoret na Karen, ikivutia zaidi ya wachezaji 4,200 wa gofu ambao wameshiriki katika mashindano, kliniki za vijana na programu za uhamasishaji.
Baada ya mchuano wa Nyali, mikondo sita zaidi itafanyika kabla ya msururu huo kukamilika kwa mchujo mkubwa katika Vipingo Ridge, Kaunti ya Kilifi, Agosti.
Safaricom pia imeshirikiana na Junior Golf Foundation kuendelea kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika mchezo huo. Vijana wanaweza kujisajili na Wakfu wa Gofu wa Junior (JGF) kwa KES.1,000 na kupata klabu yoyote ya gofu nchini.