Shirika la Afya duniani (WHO) kwa ushirikiano na kaunti ya Mombasa limezindua mpango wa ushiriki wa jamii kwenye vita dhidi ya ugonjwa wa Covid 19.
Kampeini hiyo inalenga kutoa uhamasisho na habari kuhusu maagizo ya serikali katika kupambana na maradhi ya Covid 19.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa magari yatakayotumika katika kampeini hiyo, Afisa wa afya ya umma kaunti ya Mombasa, Aisha Abubakar, amesema mpango huo utahusisha kaunti ndogo sita za Mvita, Likoni, Changamwe, Kisauni, Nyali na Jomvu ambapo kila moja itakabidhiwa magari mawili.
Mwenyekiti wa United Front, Said Mabrouk, ambaye shirika lake linashirikiana na hospitali ya MEWA katika kampeini hiyo,amedokeza kuwa shirika hilo litatoa mafunzo kwa jamii katika kaunti hizo ndogo kila wiki likilenga vijana, makundi ya kina mama na watu wenye ushawishi kwenye jamii.
