Baadhi ya mashirika ya akinamama wanaotetea haki za binadamu jijini Mombasa wameeleza wamefurahishwa na hatua ya muungano wa Azimio kumchagua kiongozi wa NARC Kenya Martha Karua kama mgombea mwenza wa mgombea urais wa chama cha Azimio la umoja one Kenya Raila Odinga.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa shirika la akinamama kuhusu uenezaji wa amani jijini Mombasa Grace Oloo wamese hii ndio fursa nzuri kwa changamoto za wanawake kuangaziwa bila pingamizi.
Kwa mujibu wa Aloo, Karua ni kiongozi shupavu na yuko na tajriba ya kipekee kuongoza taifa, hivyo akawahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Kwa upande wake afisa mtetezi wa haki za binadamu katika shirika la kutetea haki za binadamu la MUHURI Topister Juma ameeleza kuwa uteuzi wa mama kwenye wadhfa wa naibu rais utawezesha haki za akinamama kutekelezwa na kusikizwa kwa urahisi na ni historia kubwa kwa taifa la Kenya.
Haya yanajiri mda mfupi baada ya kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kumtangaza kiongozi wa NARC Kenya Martha Karua kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu tarehe 9 mwezi Agosti.