Wabunge sasa wanataka mpango wa Kazi Mtaani uliozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta kusitishwa wakisema ulipangwa vibaya na ni njia tu ya kufuja fedha za umma.
Wakizungumza jana wakati wa siku ya pili ya mkutano wa tatu wa Bunge la Kitaifa, wabunge hao walilalamika kwamba vijana wengi hususan katika maeneo bunge wamefungiwa nje ya mpango huo.
Wabunge Peter Mwathi wa Limuru, naibu spika Moses Cheboi na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Urasimu ya bunge la kitaifa, Kanini Kega wamesema mradi huo si endelevu na kuna haja ya mabadiliko.
Hata hivyo waziri wa fedha Ukur Yattani ameweka wazi kuwa mpango huo utaendelea hadi mwisho wa mwaka kama ilivyokusudiwa ili kuwasaidia vijana kifedha kutokana na athari za covid-19.
Kufikia sasa serikali imetumia kima cha shilingi bilioni 1.3 katika awamu ya kwanza ya Kazi Mtaani huku ikitenga shilingi bilioni 2.4 na bilioni 5.6 kutumika katika awamu ya pili na tatu.