Wafanyibiashara katika eneo la Diani kaunti ya Kwale wamefanya mandamano ya amani kulalamikia hatua ya serikali ya kaunti hiyo kubomoa vibanda vyao vya biashara.
Wafanyibiashara hao wanaouza vinyago na bidhaa zingine kwa watalii wamepinga vikali hatua hiyo inayolenga kutoa nafasi kwa mradi wa ujenzi wa mabomba ya kupitisha maji katika eneo hilo.
Wakiongozwa na Mike Musili, wafanyibiashara hao wamedai kutopewa ilani ya kuondoka na serikali ya kaunti hiyo.
Sasa wafanyibiashara hao wanaitaka serikali ya kaunti kuwalipa fidia ya hasara ya mali yao kwani wanategemea biashara hizo kujikimu kimaisha.
Aidha, wamemtaka gavana wa kaunti hii Salim Mvurya na mbunge wa eneo hilo kuingilia kati ili kuona kwamba zoezi hilo linasitishwa.
Hata hivyo, mkurugenzi wa kampuni ya usambazaji maji Kwale (KWAWASCO) Eric Parmet ameahidi kuwa wafanyibiashara walioathirika watafidiwa.