Jaji Mkuu Martha Koome amewaonya wazazi wenye tabia ya kushtaki walimu na shule baada ya watoto wao kufukuzwa kwa kuvunja sheria za shule kuwa kesi hizo zitatupiliwa mbali na wazazi kuwajibikia kwa gharama.
Akizungumza leo katika Shule ya Upili ya wasichana ya Loreto Limuru katika Kaunti ya Kiambu, Koome amesema kuwa aina zote za utovu wa nidhamu haziwezi kuvumiliwa na kwamba lazima wazazi wawajibike kuwalea watoto wao kwa maadili.
Kama njia mojawapo ya kuhakikisha kwamba watoto wanalindwa kikamilifu, CJ Koome alipendekeza kuboreshwa kwa sheria za ulinzi wa watoto, akionya kwamba washukiwa wote watakaopatikana na hatia ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto watakabiliwa na kifungo cha angalau miaka 20 jela.