Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini (EACC), imewasilisha kesi mahakamani kutaka mali ya thamani ya shilingi million 278 ya afisa wa zamani wa halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini -KRA kutwaliwa na serikali.
Tume hiyo inasema imekamilisha uchunguzi na kubaini kwamba kati ya mwezi Januari mwaka 2012 na Januari mwaka 2021, afisa huyo Jeremiah Kinyua alijipatia utajiri usioambatana na mapato yake.
Mnamo mwezi Oktoba mwaka 2021, mahakama ilitoa maagizo ya miezi sita, kuzuia uuzaji wa mali za afisa huyo zenye thamani ya shilingi million 192 na pia gari lake lenye thamani ya million tano.
Sasa tume ya EACC inataka mali hizo ambazo thamani yake imeongezeka kurejeshwa kwa serikali.
Uchunguzi wa tume hiyo umebaini kwamba, Kinyua alipokea kiasi kikubwa cha pesa kupitia akaunti mbali mbali za Benki ambazo chanzo chake hakijabainika.
Tume hiyo inashuku kwamba pesa hizo zilikuwa za rushwa iliyotolewa kwa Kinyua kuambatana na majukumu yake katika halmashauri ya KRA.
Siku ya Alhamisi, Jaji Esther Maina alitoa maagizo ya kumzuia Kinyua kustawisha ama kuuza vipande vitano vya ardhi vya thamani ya shilling million 69.