Ajali Mbaya Zaidi Kuwahi Kutokea Kwenye Maandalizi ya Filamu

Kiwanda cha filamu cha Hollywood nchini Marekani, huchukuliwa kuwa cha kale zaidi ulimwenguni kwa sababu huko ndio studio za kwanza za kuandaa filamu na kampuni za kuandaa filamu zilianzia. Kwa sababu hiyo kimekuwa sana na maandalizi ya filamu huko ni tofauti na ya barani Afrika labda kwa jinsi waandalizi hujaribu sana kuhakikisha kwamba kazi wanazoandaa zinakaribia ukweli. Matukio kama ajali, moto na mengineyo wakati mwingine hutekelezwa kikweli na hata silaha kama bunduki huwa za kweli. Katika mazangira hayo, ajali zinaweza kutokea na ndio sababu tunaangazia ajali mbaya zaidi katika historia ya maandalizi ya filamu ulimwenguni.

Ajali ya hivi punde zaidi katika maandalizi ya filamu ilitokea mwaka 2021 hususan mwezi Oktoba. Bi. Halyna Hutchins ambaye ni mwelekezi wa shughuli ya kupiga picha na kunakili video alifariki kutokana na majeraha ya risasi ambayo ilimpata wakiendelea kuandaa filamu kwa jina “Rust”. Tarehe 21 mwezi Oktoba mwaka jana, mzaliwa huyo wa Ukraine alikuwa kazini na wenzake katika eneo la “La Cienega”, New Mexico, nchini Marekani ambapo mwigizaji Alec Baldwin alifyatua risasi kutoka kwenye bunduki ambayo alifaa kutumia katika maigizo na kusababishia majeraha Halyna na mwelekezi Joel Souza. Halyna aliaga dunia baadaye akipokea matibabu hospitalini na keshoye, Baldwin akatoa taarifa akionyesha mshtuko.

Also Read
Mimi Mars nyumbani kwa Diamond!

Baadaye ilibainika kwamba bunduki za kutumiwa katika uigizaji hazifai kuwa na risasi na kwa sasa familia ya mwendazake Hutchins imemshtaki Baldwin na wahusika wengine kortini ikisema kifo chake kilitokana na utepetevu na haja ya kupunguza gharama. Mwili wa Halyna ulizikwa katika makaburi ya Hollywood Forever katika eneo la Hollywood, California.

Ajali nyingine ni ya mwaka 1982, kwenye maandalizi ya filamu kwa jina “The Twilight Zone” ambayo inasemekana kubadili jinsi filamu huandaliwa. Mwigizaji Vic Morrow na watoto wawili waigizaji walikufa kwenye ajali ya ndege iliyokuwa ikitumiwa kuandaa filamu baada ya ndege hiyo kuanguka. Mwili wa mtoto Renee Chen uliharibiwa kabisa huku ile ya Morrow na Myca Dinh Le ikikatwa na mabati ya ndege. Ilistahili kutokea kama ajali ambayo inakaribia kutokea ya ndege na Morrow alikuwa aseme maneno, “Nitahakikisha mko salama, ninaahidi. Hakuna kitakachowadhuru, naapia Mungu” maneno ambayo hakufika kusema.

Mwaka 1986 Art Scholl, mwendesha ndege na ambaye alifahamu vyema mbwembwe za uendeshaji ndege kama vile kuizungusha ikiwa hewani alitumbukia bahari ya Pacific baada ya kushindwa kuidhibiti ndege huku akinakili picha kwenye maandalizi ya filamu “Top Gun”. Alikuwa amewahi kuhudumu kwenye filam kama vile “The Right Stuff”, “Iron Eagle”, na “Indiana Jones and the Temple of Doom”. Mwili wa Scholl haukuwahi kupatikana.

Also Read
Tiffany Haddish apendekezwa kuchukua mahala pa Ellen DeGeneres

Brandon Lee, mwanawe Bruce Lee, aliaga kwenye maandalizi ya filamu “The Crow” ya mwaka 1994 ilipofika sehemu ya kuigiza kwamba amepigwa risasi. Bunduki iliyotumika wakati huo inasemekana kutosafishwa vyema ingawa haikuwa na risasi. Kilichosababiisha kifo cha Brandon, ni mkusanyiko wa mabaki ya maganda ya risasi ambayo yalifyatuka na kumpata kifuani. Alikimbizwa hospitalini ambapo alikata roho kutokana na kuvuja damu kwa wingi.

George Clooney mwigizaji nguli wa filamu za Marekani na ambaye pia ni mtayarishi amesalia na makovu kutokana na majeraha aliyoyapata mwaka 2005 wakati ajali ilitokea wakiendelea kuandaa filamu kwa jina “Syriana”. Alikuwa akiigiza sehemu moja ambapo amefungwa kwenye kiti huku akichapwa ambayo walirudia mara nyingi ili kuipata vizuri. Katika hali hiyo alijeruhiwa wakati alichapwa sana, kiti kile kikasukumwa na akagongwa kichwa. Alipohojiwa, Clooney ambaye ana umri wa miaka 61 alisema kwamba nyama ambayo inazingira uti wa mgongo ilidhurika kwenye ajali hiyo. Majeraha yake hayakuchukuliwa kwa uzito mwanzo mwanzo lakini kadri siku zilivyoendelea kupita ndipo maumivu yalimzidia hasa ya kichwa. Alitafakari kujitoa uhai mara nyingi lakini baada ya kufanyiwa upasuaji zaidi ya mara moja, matumaini yakarejea na jukumu lake kwenye filamu hiyo ya Syriana likamshindia tuzo ya mwigizaji bora msaidizi.

Also Read
Tiffany Haddish kurudia vazi lake kwa mara ya tisa!

Katika maandalizi ya filamu ya mwaka 2008 inayofahamika kama “The Dark Knight” Conway Wickliffe aliaga dunia kwenye ajali ya gari wakati alikuwa akijifundisha jinsi angetekeleza jukumu la ajali.

Sarah Jones ambaye alikuwa msaidizi wa mpiga picha kwenye maandalizi ya filamu ya mwaka 2014 kwa jina “Midnight Rider: The Gregg Allman Story” aliaga dunia kutokana na ajali ya treni. Ilikuwa siku ya kwanza ya maandalizi ya kazi hiyo ya sanaa na walikuwa wakiifanya katika barabara ya reli ambayo ilikuwa ikitumika. Alipatiwa onyo la chini ya dakika moja kuondoka kwenye reli na hakufanikiwa kumaliza kuondoa vifaa vyao na gari moshi lilipokuja likamuua.

Mwigizaji Dylan O’Brien alipata majeraha wakati wakiandaa filamu ya “Maze Runner” cha mwaka 2016, alikuwa akiigiza sehemu ambayo ilimhitaji atembee akiwa juu ya paa la gari moja lililokuwa likienda hadi juu ya gari jingine ambalo pia lilikuwa kwenye mwendo akakosa kufikia la pili vizuri akaanguka na kuburutwa chini ya gari. Majeraha yake yalisababisha maandalizi ya kazi hiyo kusimamishwa kwa mwaka mmoja ili apate nafuu ndipo waendelee. Maze Runner: The Death Cure mwishowe ilizinduliwa mwaka 2018. Hizo ni baadhi tu ya ajali ambazo zimenakiliwa za maandalizi ya filamu.

  

Latest posts

Kourtney Kardashian na Travis Barker wafunga ndoa kwa mara ya tatu

Tom Mathinji

Wimbo mpya wa Bahati wapata ufuasi wa watu milioni moja

Tom Mathinji

Wizkid asema albamu yake mpya imekamilika

Tom Mathinji

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi