Mwanamuziki wa Uganda AK 47 ambaye jina lake halisi ni Emmanuel Mayanja atakumbukwa hii leo kupitia misa ambayo imeandaliwa na watu wa familia yake, miaka saba tangu aiage dunia. Misa hiyo ambayo itaandaliwa leo katika eneo la Kalangaro wilaya ya Mityana nchini Uganda ni mojawapo ya mipango ya mwaka huu ya kukumbuka mwanamuziki huyo wa mtindo wa Dancehall. Familia ya Mayanja imealika mashabiki wa marehemu kwa misa hiyo.
AK 47 aliaga dunia punde baada ya kufikishwa katika hospitali ya Nsambya tarehe 16 mwezi Machi mwaka 2015 kutokana na majeraha aliyoyapata kufuatia kuanguka kwenye choo cha sehemu moja ya burudani iitwayo Dejavu katika eneo la Kansanga. Utata umeghubika kifo cha kutatanisha cha mwanamuziki huyo huku kukiwa na ripoti kinzani kuhusu kilichomuua.
Siku yake ya mwisho ulimwenguni, mwanamuziki huyo alirekodi wimbo uitwao “Ndi Mulokole” ambao unamaanisha “Nimeokoka”. Baadaye akaandika kwenye Facebook maneno haya, “Nze Ndi Mulokole Nafuuka Mulokole AK Mulokole Naawe Fuuka Mulokole In God we trust” yaani “Nimeokoka, nimepokea wokovu, AK mwokovu, nawe pia okoka, Tunaamini Mungu”.
Saa mbili usiku akakwenda kwenye sehemu ya burudani iliyokuwa ikimilikiwa na meneja wake Bwana Jeff Kiwa jijini Kampala ambapo alishiriki vinywaji na marafiki. Saa nne usiku huo huo alipatikana amezirai chooni huku akitokwa damu kwenye mapua.
Kabla ya kifo chake, kaka huyo mdogo wa Jose Chameleone, Pallaso na Weasel ambao wote ni wanamuziki, alikuwa amesajiliwa na kampuni ya muziki ya “Team No Sleep – T.N.S” na alikuwa amegundua uwezo wake katika muziki kiasi cha kupendelewa sana na mashabiki.
Aliacha watoto mapacha ambao alizaa na mpenzi wake Nalongo Maggie Kiweesi. Maggie aliolewa mwaka uliopita wa 2021 na mmoja wa marafiki wa karibu wa marehemu AK 47, ambaye anaitwa Sseguya Faisal au ukipenda Rabadaba.