Akothee azua mjadala mitandaoni

Mwanamuziki na mfanyibiashara Esther Akoth maarufu kama Akothee amezua gumzo mitandaoni kuhusu wanaume ambao wanategemea wanawake.

Alianza kwa kushangaa jinsi wanaume wamejizoesha tabia ya kukubali kulipiwa ada mbali mbali na kina dada huku akionya wanawake wawe macho zaidi na mtindo huo ambao umeshika kasi ulimwenguni kwa sasa.

Mwanamuziki huyo aliomba msamaha kwa mashabiki wake ikiwa maneno yake yaliwakwaza na kuendelea kutilia mkazo akisema ili mwanaume achukuliwe kuwa mwanaume kamili, lazima awe jawabu na wanawake ni wasaidizi tu.

Kulingana naye, hamna tatizo ikiwa mume hana kazi na mke ana kazi ila tatizo linaanza pale ambapo mwanaume anatosheka na ufukara wake na anategemea mke kwa kila jambo.

Akothee ambaye pia hujiita Madam Boss ameonya kina dada dhidi ya kuchukua mikopo mikubwa na kukabidhi wanaume pesa hizo. Visa vya kina dada kutapeliwa pesa nyingi na wapenzi wao vimeongezeka sana duniani kote lakini Akothee anahimiza wote ambao wamekumbana navyo kutokufa moyo ila wajiendeleze maishani huku wakiwa waangalifu zaidi.

Alipoulizwa kuhusu mume ambaye amepoteza ajira, Akothee alisema kuna tofauti kati ya mtu kama huyo na yule ambaye ameamua kuketi tu alishwe na mke wake. Alisema ikiwa mume amepoteza nafasi ya kazi, mke wake anastahili kumsaidia na huo ndio uzuri wa ndoa ambapo wote wanafaa kusaidiana kunapotokea jambo.

Jambo ambalo alisisitizia kina dada ni kufahamu tofauti kati ya mume na mpenzi kabla ya kuchukua hatua za kusaidia mtu kifedha.

Wakenya maarufu kama vile mwanamuziki Wahu Kagwi, Teacher Wanjiku ambaye ni mchekeshaji na Lilian Muli mtangazaji wa runinga walijibu maneno ya Akothee ambapo walionekana kumuunga mkono.

Baadhi ya mashabiki wake wa kiume wanaonelea kwamba anapotosha kina dada wa Kenya.

  

Latest posts

Harusi ya Nandy Kuwa ya Awamu Tatu

Marion Bosire

Mwigizaji Mkongwe wa Nollywood Kenneth Aguba Apata Usaidizi

Marion Bosire

Travis Baker Arejea Kazini

Marion Bosire

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi