Gavana anayeondoka wa kaunti ya Machakos, Alfred Mutua, amekanusha ripoti kwamba anawania kiti cha ubunge cha Mwala.
Kupitia ujumbe wa Twitter, kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap alifafanua kwamba hatagombea kiti chochote cha uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa Agosti tarehe tisa.
“Ili kuondoa wasiwasi wowote, ningependa kufafanua kwamba, wakati huu sitawania wadhifa wowote wa kisiasa katika uchaguzi mkuu wa tarehe tisa mwezi Agosti. Ninajihusisha na kampeni za Kenya Kwanza ili taifa hili lipate mfumo mpya ili ndoto ziweze kuafikia,” alisema Mutua kupitia mtandao wake wa twitter.
Mutua alisema kuwa wakati huu anajikita katika kampeni ya muungano wa Kenya Kwanza ili Kenya ipate mfumo mpya wa uongozi.
Mapema mwezi huu, Mutua alijiondoa kutoka Muungano wa Azimio La Umoja – One Kenya na kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto, akitaja hali ya kutoaminiana katika muungano wa Azimio La Umoja – One Kenya.
Gavana huyo ambaye ameizima azma yake ya kuwania Urais, alifichua kuwa alikuwa amejadiliana na wakuu wa muungano wa Kenya Kwanza ili kupewa nafasi kubwa iwapo muungano huo utashinda uchaguzi