Mwanamuziki wa Marekani Brandon Paak Anderson maarufu kama Anderson .Paak ametumia ngozi ya mkono wake kama bango la kutoa ilani. Paak wa umri wa miaka 35 alichora tatoo ya maneno ambayo yanaonya dhidi ya kazi yake yoyote ya muziki kuzinduliwa baada ya kifo chake.
Kulingana naye kazi ambazo zitakuwa hazijatoka rasmi kwa umma kufikia siku ya kifo chake ni kazi za mwanzo tu ambazo hazifai kutolewa kwa umma kwa vyovyote vile.
Ameandika maneno hayo kwenye mkono wake kwa lugha ya kiingereza, “When I’m gone please don’t release any posthumous albums or songs with my name attached, those were just demos and never intended to be heard by the public.”
Hatua ya Paak huenda inatokana na mtindo ambao unaendelea kwa sasa wa watayarishi wa muziki kutoa kazi za wasanii ambao wameshaaga dunia ambao walikuwa chini ya usimamizi wao.
Wanamuziki ambao kazi zao zimezinduliwa baada yao kufariki ni pamoja na Pop Smoke, Mac Miller, Selena, DMX, Aaliyah, Juice WRLD na Prince.
Kazi ya marehemu Prince ya “Welcome 2 America” iliandaliwa mwaka 2010, akaaga dunia mwaka 2016 na imetolewa rasmi mwisho wa mwezi Julai mwaka huu wa 2021, miaka 11 tangu iandaliwe.