“Leo sitalia, niko na furaha.” ndiyo maneno ambayo mwanamuziki Kevin Bahati Kioko aliyasema kwenye kikao na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama cha Jubilee jana baada ya kupokezwa upya cheti cha chama hicho ili awanie kiti cha ubunge katika eneo la Mathare, kaunti ya Nairobi. Mwanamuziki huyo alikuwa amezingirwa na viongozi kadhaa wa chama hicho akiwemo katibu mkuu Mheshimiwa Jeremiah Kioni.
Tarehe 25 mwezi Aprili mwaka huu, mwanamuziki huyo ambaye anamiliki kampuni ya EMB Records, aliandaa kikao na wanahabari ambapo alitiririkwa machozi akielezea kwamba alikuwa ameshauriwa kutupilia mbali azma ya kuwania kiti hicho cha ubunge eneo la Mathare. Bahati alimsihi kiongozi wa chama cha Jubilee Rais Uhuru Kenyatta apatie vijana fursa ya kuongoza. “Hiki cheti sio tu cha Bahati, ni cha vijana wote wa Mathare. Watu wa Mathare wanahitaji kiongozi ambaye anaelewa shida zao na ambaye ameishi nao.” alisema mwimbaji huyo kuhusu cheti alichokabidhiwa siku tatu zilizokuwa zimepita.
Bahati alizaliwa na kulelewa eneo la Mathare katika makao ya watoto yatima baada ya mamake kuaga dunia.
Katika kikao cha hicho cha mwezi jana, Bahati alisema kwamba anafahamu makubaliano yaliyoafikiwa na viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja Kenya Kwanza ambapo kila chama kimepatiwa eneo bunge la kuongoza katika kaunti ya Nairobi. Kulingana naye chini ya makubaliano hayo eneo bunge la Mathare lilikuwa limeachiwa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.
Wito wake unaonekana kuridhiwa na viongozi wa Muungano wa Azimio ambapo sasa ana cheti rasmi. Alitoa shukrani kwa Mungu kwa kujibu maombi, na kwa viongozi wa muungano huo wa kisiasa kwa kusikia kilio chake.