kaimu gavana wa Jiji Nairobi Ann Kananu, akiwa ameandamana na Waziri wa barabara Mohamed Dagane, siku ya Alhamisi walizindua barabara kwa jina Francis Atwoli katika mtaa wa Kileleshwa.
Barabara hiyo ambayo awali ilijulikana kama Dik Dik, ilipewa jina jipya Francis Atwoli baada ya mtetezi maarufu wa wafanyikazi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa barabara hiyo naibu Gavana wa Nairobi ambaye pia ni Kaimu gavana wa Nairobi Ann Kananu, alisema jina hilo jipya ni kwa heshima ya mchango muhimu Atwoli wa kupigania haki ya wafanyikazi hapa nchini kwa muda wa miaka 54.
Atwoli alimshukuru naibu huyo Gavana na bunge la kaunti ya Nairobi kwa kuipa barabara hiyo jina lake.
Mwaka huu barabara ya Accra ilipewa jina jipya la Kenneth Matiba nayo barabara ya Eastleigh First Avenue ikapewa jina la Yusuf Hajji.
Mwaka 2016, barabara ya Forest Road ilibadilishwa jina na kupewa Wangari Maathai huku Ile ya Cross Road ikipewa jina la Charles Rubia.