Barabara kuu ya Uhuru- Waiyaki iliyoathirika na ujenzi wa barabara mpya ya juu kwa juu,itafunguliwa upya tarehe 25 mwezi disema mwaka huu.
Waziri wa barabara na uchukuzi James Macharia alitangaza hayo hii leo akisema kuwa sehemu kadhaa za barabara hiyo zilizokuwa zimefungwa tayari zimefunguliwa kwa umma.
Akiongea wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara hiyo ya juu kwa juu ambayo asili mia 75 ya ujenzi wake umekamilika,waziri alisema sehemu ya makutano ya barabara hiyo ya Westlands / James Gichuru ilifunguliwa siku ya ijumaa .
Alisema kuwa mzunguko wa magari wa Haile Selassie–University Way unatarajiwa kufunguliwa tarehe 15 mwezi disemba.Barabara hiyo ya juu kwa juu ya umbali wa kilomita 27 itagharimu shilingi bilioni 62 itakapo kamilika.
Wenye magari watahitajika kulipa ada kutumia barabara hiyo kutoka Mlolongo hadi makutano ya James Gichuru huko Westlands.
Barabara hiyo itachukua wenye magari dakika 20 pekee kufika makutano ya James Gichuru kutoka Mlolongo na watumiaji watalipia ada ya kati ya shilingi 200 na 300, itakayotumiwa kuikarabati na kuiweka katika hali shwari.