Sofapaka watazindua uhasama wa jadi na mabingwa watetezi wa ligi kuu Kenya, Tusker FC katika mchuano wa pekee Ijumaa katika uwanja wa Wundanyi,kaunti ya Taita Taveta, huku ligi kuu ya Kenya ikirejea kwa mechi za raundi ya 19 , baada ya mapumziko wiki iliyopita.
Sofapaka maarufu kama Batoto Ba Mungu walirejelea tambo za ushindi walipoikwatua Wazito Fc mabao 2-1 ,wiki mbili zilizopita , wakati wagema mvinnyo Tusker wakiambualia sare dhidi ya wanajeshi Ulinzi Stars.
Katika msuururu wa mechi 4 za mwisho,Sofapaka wameshinda pambano moja na kurekodi sare tatu, wakikalia nafasi ya 10 ligini kwa alama 24, huku Tusker wakishinda mechi tatu kati ya nne za mwisho na kuzoa jumla ya alama 30 ,matokeo yanayowaacha katika nafasi ya 6 kwenye jedwali.
Timu hizo zitakutana kwa mara ya 21 katika historia , Sofapaka wakishinda mechi 10 ,Tusker wakashinda 6 na michuano minne kumalizikia sare na jumla ya mabao 30 yakifungwa .
Pambano hilo litasakatwa katika uwanja wa Kasarani Annex.