Wanafunzi 50 waliofanya vizuri kwenye mtihani wa kitaifa wa shule za upili (KCSE) wa mwaka 2020 watapata nafasi ya kujiunga na mpango wa uanagenzi chini ya Wakfu wa Benki ya KCB kabla ya kujiunga na vyuo vikuu.
Miongoni mwao ni Allan Udoma kutoka Shule ya Upili ya Agoro Sare huko Oyugis, ambaye aliibuka wa pili bora kitaifa kwenye mtihani huo.
Wanagenzi hao watahudumu kwa miezi mitatu kwenye tawi la Benki ya KCB lililo karibu nao.
Wanafunzi 200 kati ya 240 wa shule za upili waliofanya mtihani wa KCSE wa mwaka 2020 chini ya ufadhili wa wakfu huo wamefaulu kujiunga na vyuo vikuu baada ya kupata alama za C+ na zaidi.
Kainmu Afisa Mkuu wa Wakfu wa KCB Caroline Wanjeri alisema wanafunzi waliofanya mtihani huo walikabiliwa na wakati mgumu kutokana na janga la korona.
Wakfu wa KCB huwasaidia takriban wanafunzi 240 wenye mahitaji na wanaojiunga na kidato cha kwanza kutoka sehemu zote za humu nchini kila mwaka, ambapo 40 kati yao huwa ni walemavu.
Wanafunzi hao hupatiwa msaada wa masomo wa miaka minne katika shule za upili za umma ambapo wanalipiwa karo, kununuliwa vitabu na sare za shule.