Umoja wa mataifa umehimiza Ethiopia, Misri na Sudan kurejelea meza ya mazungumzo yanayo-ongozwa na muungano wa Afrika ili kumaliza mzozo kuhusu mradi wa bwawa kubwa la maji ambalo linajengwa na Ethiopia, kwenye mto Nile.
Katika taarifa yake umoja huo ulihimiza mataifa hayo matatu kuafikia makubaliano ya kudumu kuhusu njia za kujaza maji kwenye bwawa hilo la kuzalisha umeme al-maarufu “The Grand Ethiopian Renaissance Dam”- kwa ufupi (GERD).
Mradi huo unao-endelea tangu mwaka 2011, unatarajwia kuzalisha Mega Watts 6,000 za umeme pindi utakapokamilika.
Hata hivyo mradi huo, haujafurahisha Misri na Sudan, ambazo pia hutegemea maji ya mto huo wa Nile.
Duru ya mwisho ya mazungumzo ilimalizika mwezi April mwaka 2021 Jijini Kinshasa bila makubaliano yoyote.
Mnamo mwezi Julai, Ethiopia ilitangaza kukamilika kwa awamu ya pili ya kujaza maji kwenye bwawa hilo, hivyo kuibua malumbano zaidi kati yake na mataifa ya Sudan na Misri.
Ethiopia inasema bwawa hilo liko karibu kukamilika na litaanza kwa kuzalisha megawatts 750 za umeme baadaye mwaka huu.