Joseph Mayanja mwanamuziki wa Uganda maarufu kama Jose Chameleone anapanga kuchukua mapumziko ya muda wa miezi mitatu kutoka kwa muziki. Jose amekuwa thabiti katika kutoa nyimbo kila wakati tangu alipoingilia fani ya muziki miaka ya 90. Ametangaza kwamba atatumia muda huo wa miezi mitatu kukaa na familia yake nchini Marekani. Hajakwenda huko tangu mwaka 2019 na sasa amepata Visa ya kusafiri huko.
Chamili, anavyoitwa na wengine, alinunua nyumba nchini Marekani kwa gharama ya dola laki mbili na akahamishia familia yake yote huko mwaka 2019. Ametamani sana kuwa na mke wake aitwaye Daniella na watoto Abba Marcus, Amma Christian, Alba Shyne, Ayla Onsea na Alfa Joseph lakini ikawa vigumu kutokana na kuchelewa kupata Visa na janga la Covid 19.
Chameleone amekuwa akiugua kiasi cha kulazwa hospitalini lakini anahakikisha kwamba anarejelea kazi ya kutumbuiza mashabiki wake jinsi anafahamu mwenyewe. Hii leo Ijumaa tarehe 13 mwezi Mei mwaka 2022, nyota huyo wa muziki anaadaa tamasha nchini Burundi, mjini Bujumbumbura katika eneo la burudani la Van Beach Resort.
Huku haya yakijiri, mwanamuziki huyo ambaye anamiliki kampuni ya muziki ya Leone Island amedhihirisha kwamba bado ana mashiko na mashabiki wake. Haya yanadhihirika kutokana na jinsi kazi yake ya hivi punde zaidi imepokelewa mitandaoni. Video ya wimbo huo uitwao “Kuuma Obwesigwa” kwenye mtandao wa You Tube ilitizamwa mara nyingi muda mfupi tu baada ya kuchapishwa. Alishukuru mashabiki wa nchi kama vile Botswana, Zambia, Malawi, Kenya, DRC, Congo, Tanzania, Mozambique na Zimbabwe ambao takwimu zinaonyesha waliongoza katika kutizama video hiyo.