Dozi za chanjo ya Covid 19 kutoka kampuni ya Johnson & Johnson ambazo hutolewa mara moja pekee sasa zinapatikana humu nchini.
Hii ni chanjo ya tatu kujumuishwa kwenye mipango ya chanjo nchini Kenya, baada ya zile za AstraZeneca na Moderna.
Shehena ya kwanza ya dozi 141,600 za chanjo ya kampuni ya Johnson & Johnson ilipokewa Ijumaa usiku kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na maafisa wa wizara ya afya wakiongozwa na katibu mwandamizi Dkt. Mercy Mwangangi.
Akiongea kwenye uwanja wa ndege wa JKIA, baada ya kuwasili kwa chanjo hizo, DKt. Mwangangi alisema dozi hizo ambazo mtu hahitaji kuchanjwa mara mbili, zitasaidia kuhakikisha kwamba wakenya ambao maisha yao yanahitaji kusafiri huku na kule, wanapata chanjo kamili.
Alisema wizara ya afya itahakikisha wakati wa kusambaza chanjo hiyo ya Johnson and Johnson kwamba inapelekwa katika ngazi za afya ya kimsingi kwa vile haina gharama nyingi kusamabzwa.
Mbali na hayo, Kenya ilipokea mchango wa dozi elfu-55 za chanjo ya AstraZeneca kutoka kwa Jamhuri ya Latvia siku ya Jumamosi ili kusaidia kukithi mahitaji ya chanjo humu nchini huku serikali ikilenga kuwapatia chanjo watu wazima million 10 itimiapo mwisho wa mwaka 2021.