Waziri wa usalama wa taifa Dkt. Fred Matiang’I ametoa wito kwa wadau katika sekta ya kibinafsi kutokubali kutishwa na kuitishwa pesa na wanasiasa walaghai wanaodai kuwa watawapa sekta hiyo ulinzi katika serikali ijayo.
Matiang’i alisema kuwa mashirika ya kijasusi yanatambua kuwa kuna baadhi ya wanasiasa walaghai ambao wanatafuta misaada ya pesa kutoka kwa wanasiasa mashuhuri wakidai kuwa watawapa ulinzi katika serikali ijayo.
Alisema kuwa misaada ya kulazimisha kupewa pesa za kufanyia kampeini si halali.
Alidai kuwa baadhi ya watu hao wanatumiwa kuvuruga mchakato wa uchaguzi kwa kukodisha wananchi na kuwahonga wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa tarehe tisa mwezi Agosti mwaka huu.
Waziri alisema kuwa serikali ina orodha ya mashirika yote ambayo yamekuwa yakiafikia mikataba usiku na wanasiasa huku akidai kuwa mengi ya mashirika hayo hukwepa kulipa ushuru.
Matiang’i wakati huo huo alisisitiza kujitolea kwa wizara yake kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa amani.
Alisema miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kununua magari mapya 2,720 ili kurahisisha usafiri na kuwezesha maafisa wa polisi kushughulikia maswala ya dharura kwa haraka.
Alitoa wito kwa watu wanaonuia kuwania nyadhifa za uchaguzi na wapiga kuwa mabalozi wa amani na kuhakikisha kuwa taifa hili linasalia dhabiti.
Matiang’i alikuwa akiongea jijini Nairobi wakati wa awamu ya tatu ya mazungumzo baina ya chama cha wadau katika sekta ya kibinafsi-KEPSA na kamati ya bunge kuhusu utekelezaji wa miradi ya kitaifa na mawasiliano.
Mkutano huo ulitayarishwa kama ule wa mikakati ya kufuatilia inayolenga ukuaji wa uchumi na biashara kabla ya uchaguzi mkuu wa tarehe tisa mwezi Agosti mwaka huu.