Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini Kenya KFCB Daktari Ezekiel Mutua ametangaza Wikendi inayoanza kesho kuwa wikendi ya Firirinda.
Kwenye ukurasa wake wa Facebook Dakta Mutua aliandika, “Nimetangaza wikendi ijayo kuanzia kesho Ijumaa hadi Jumapili kuwa wikendi ya Firirinda kwa heshima yake na kwa ajili ya kusaidia mwandishi na mwimbaji wa wimbo huo ambaye anaugua Mzee Dickson Munyonyi. Wapiga muziki kwenye hafla zote za wikendi hii wanaombwa wacheze wimbo huo na kuhimiza mashabiki wao kuchanga fedha za kusaidia kulipa ada ya hospitali ya mwanamuziki huyo mkongwe ambaye anaendelea kupokea matibabu. Nambari ya kutuma fedha hizo kwa njia ya simu itatangazwa baada ya sisi kuwasiliana na familia na mimi nitaanzisha mchango kwa shilingi laki moja. Tuujulikanishe wimbo huu lakini zaidi na la maana ni kuutumia kusaidia mwimbaji wake ambaye anatupa kumbukumbu huku tukisherehekea utamaduni wetu.”
Dakta Mutua anasema changamoto ya Firirinda kwenye mitandao ya kijamii inafaa kuchukua mahala pa ile ya Jerusalema!
Alitumia nafasi hiyo pia kuomba yeyote ambaye anafahamu familia ya mzee huyo awasiliane naye ili amuunganishe nayo.
Kulingana na Mutua, Firirinda ni neno ambalo linatokana na maneno mawili Free la kiingereza na Rinda la kiswahili kuashiria vazi la kike.