Mwigizaji mkongwe wa filamu za nchini Nigeria almaarufu Nollywood Bwana Richard Gbenga ameaga dunia. Taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaashiria kwamba Gbenga alikata roho asubuhi ya alhamisi tarehe 12 mwezi Mei mwaka 2022. Richard, ambaye wakati mmoja alikuwa mwigizaji stadi, anasemekana kuwa fukara na alikuwa hawezi kulipia hata matibabu yake. Inasemekana mzee huyo alikuwa aliugua kisukari na magonjwa mengine ambapo mwaka jana marafiki wake walimchangia fedha za kugharamia matibabu.
Miaka ya 90, Richard alitesa anga na uigizaji wake. Alihusika kwenye filamu kama vile Sango, Mirror in the sun, 30 Days, Darkest Night, na Betrayal of Love, kati ya nyingine nyingi. Watayarishaji filamu walipenda sana kumpa majukumu ya kupigana au kutisha kutokana na sauti yake nzito na kimo chake. Wakati mmoja kwenye mahojiano, mwigizaji huyo alisema kwamba anahisi watayarishaji filamu hawajatumia uwezo wake wa kuigiza kikamilifu na kwamba kati ya kazi zake za awali hawezi kuchagua moja akasema ndiyo nzuri zaidi.
Mwezi Mei mwaka jana Gbenga alichapisha picha yake akisema anaendelea kupata nafuu. Mwezi Juni mwaka huo, alitambuliwa kwenye tuzo za “National Royal Awards” kama mwigizaji bora wa kiume wa mwaka.
Kuhusu ndoa, Richards alikuwa ameoa mwigizaji mwenza kwa jina Florence, ndoa ambayo inasemekana kusambaratika mwaka 2019. Ana mtoto wa kiume kwa jina Richards Ikye Isaiah ambaye anamfanana sana na alikuwa anapenda sana kuchapisha picha zake kwenye mitandao ya kijamii.