Miamba Gor Mahia na AFC Leopards watatumia jezi mpya za msimu wa mwaka 2021/2022 kuanzia wikendi hii .
Timu hizo mbili zinazofadhiliwa na kampuni ya Betsafe zilizundua sare za msimu siku ya Jumatatano .
Wasimamizi wa timu hizo mbili waliwarai wadhamini wao ,Betsafe kuongeza kiwango cha pesa za ufadhili baada ya kupunguza kwa asilimia 20 Julai mwaka huu, kufuatia hatua ya serikali ya kuanza kutoza ushuru wa ziada kwa kampuni za kamari.

“Hali imekuwa ngumu kuendesha timu,lakini nawashuruku wadhamini wetu kwa kusimama nasi kile tunaomba ni kwa wao kufukiria upya kuongeza kiwango cha ufadhili baada ya kupunguza Julai mwaka huu”akasema mwenyekiti wa Gor Mahia Dan Shikanda
Kwa upande wake afisa mkuu mtendaji wa Gor Mahia Raymond Oruo amesema wanalenga kuendelea kusajili matokeo bora msimu huu kuanzia kwa mchuano wa ligi kuu dhidi ya Kakamega Homeboyz.
“Sisi tunalenga kudumisha msururu wa matokeo mazuri msimu huu,tulitoka sare na Bandari Fc lakini tunatumai tutafanya vyema dhidi ya Kakamega Homeboyz”akasema Oruo
Kampuni ya Betsafe ambayo hufadhili timu hizo mbili imeahidi kuendelea kuzisaidia timu hizo ,licha ya hali ngumu ya kiuchumi kwa mjibu wa CEO wa Betsafe Victor Simiyu.
” Tumekuwa na hali ngumu ya kiuchumi ,lakini sisi tutaendelea kusimama na nyinyi kwa kila hali”akasisitiza Simiyu
Timu hizo mbili zitaanza kutumia sare zao mpya kuanzia wikendi hii,Gor wakiwa ugenini Jumamosi dhidi ya Kakamega Homeboyz wakati Ingwe wakiwa wageni wa FC Talanta.