Mwanamuziki wa Tanzania H. Baba anasema kwamba bado hajalipwa na mwanamuziki mwenza Harmonize kutokana na mchango wake kwenye kibao cha “Attitude” ambacho yeye na Awilo Longomba walishirikishwa. Mwanamuziki huyo ambaye pia ni mwanabiashara, amechapisha picha ya mvulana ambaye amevaa shati tao lililochanika na kuandika, “Haya ndiyo maisha nilikulia, ukinidhulumu haki yangu, ukadhulumu jasho langu, unanikosea. kwa hili sihitaji viherehere wa utetezi, napigania jasho langu sijamuomba pesa yake..”.
H. Baba anamsihi Harmonize ambaye anamrejelea kama mdogo wake, amlipe pesa zake kwani dhuluma ni mbaya huku akimkumbusha kwamba yeye ni tofauti na Prince Dully Sykes ambaye anadai alimdhulumu katika uwanja wa ndege. “Nipe haki yangu siogopi uwongo wako unaoutimia kwa watanzania eti unaonewa wakati unaonea kaka zako. Tukae kimya? Hapana! Nilipe mdogo Angu…” ameendelea kusema kwenye ombi hilo.
Wimbo wa “Attitude ulizinduliwa yapata mwaka mmoja uliopita na kwenye mtandao wa You Tube, umetizamwa zaidi ya mara milioni 15 na hivyo kumaanisha kwamba unaletea mwenyewe mapato. Harmonize ndiye ameuweka kwenye akaunti yake. Harmonize hajasema lolote kuhusu madai ya H.Baba ila anaangazia sana kutafuta kusamehewa na kurejelewa na mpenzi wake wa awali Frida Kajala.
Wakati fulani H.Baba ambaye alikuwa anachukuliwa kuwa mwendani wa karibu sana wa Harmonize alianza kumsifia Diamond Platnumz kwenye Instagram jambo ambalo lilishangaza wengi. Alifafanua wakati huo kwamba yeye sio kijakazi wa mtu ila anasifia mazuri.