Konde Boy, Teacher, Jeshi au ukipenda Tembo ni majina anayotumia mwanamuziki wa Tanzania Rajab Abdul Kahali maarufu kama Harmonize. Mwimbaji huyo anaendelea ziara yake kama mwanamuziki nchini Tanzania na nje ambayo inafahamika kama “Afro East Carnival” na inasheheni matamasha katika maeneo tofauti nchini Tanzania. Eneo la kwanza ambalo alizuru ni Tabata mnamo tarehe 5 mwezi Machi mwaka huu wa 2022. Baadaye Harmonize alizuru Kenya hususan Nairobi na Mombasa na sasa ni zamu ya Dar Es Salaam.
Tamasha hilo limepangiwa kufanyika tarehe 29 mwezi huu wa Mei katika uwanja wa Uhuru. Mwanamuziki huyo ambaye anamiliki kampuni ya muziki ya Konde Music anasema kujaza uwanja huo wa michezo na mashabiki ni ndoto yake sawa na ilivyo ndoto ya vijana wengi. Amesema kwamba zamu hii hachapishi picha na majina ya wasanii watakaotumbuiza ila itakuwa wakati wa wanamuziki walio chini ya Konde Music kutamba. “Huuu Ni Wakati Wa KONDEGANG F.C Mtaani Huko Kutamba Na Kuwaringishia Nguvu Ya Chama Lenu la konde gang. Ni wakati Wakuringishia Nguvu Ya Mashabiki Zangu Mtaaniiiiiii Hakuna Jina Litakalo Tajwa Kuelekea Tarehe 29/5/ PALE UHURU STADIUM zaidi Ya KONDEBOY TEACHER JESHI TEMBO BAKHRESA” ameandika Harmonize.
Anahimiza mashabiki zake wa Dar es Salaam wawe ange kujipatia tiketi za tamasha ambazo zinauzwa kwa shilingi elfu tatu pesa za Tanzania kwani anahisi zitakwisha haraka.