Taifa la Israel limetangaza sheria za hali ya hatari katikati ya mji wa Lod huku mapambano kati ya wanajeshi wa taifa hilo na Wapalastina yakiongezeka.
Magari kadhaa yaliteketezwa na watu 12 wakaripotiwa kujeruhiwa kwenye vurugu zilizotokea katika mji huo.
Wapiganaji wa Kipalastina walirusha makombora 500 ndani ya Israel, huku Israel ikijibu kwa kushambulia maeneo ya Wapalastina huko Gaza wakitumia ndege za kivita.
Iliarifiwa kuwa watu 31 wameuawa kwenye mapambano hayo ambayo ni mabaya zaidi kuwahi kutokea katika sehemu hiyo katika miaka ya hivi majuzi.
Siku ya Jumanne, Wapalastina walisema walirusha makombora 13 dhidi ya mji wa Israel wa Tel Aviv.
Wanajeshi wa Israel walisema walikuwa wakilenga wanamgambo wa Kipalastina huko Gaza, baada ya wapiganaji hao kurusha makombora dhidi ya mji wa Jerusalem na maeneo mengine.
Mapambano hayo yanajiri wiki kadhaa baada ya hali ya mvutano kujitokeza kati ya polisi wa Israel na waandamananaji wa Kipalastina kwenye maeneo matakatifu kwa waumini wa Kiislamu na Wayahudi.
Jamii ya kimataifa imezitaka pande husika kwenye mzozo huo kuukomesha.
Mjumbe wa Umoja wa mataifa huko Mashariki ya Kati Tor Wennesland amesema huenda vurugu hizo zikasababisha vita kamili.