Je, unafahamu utaratibu wa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao?

Huku taifa hili likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu tarehe tisa mwezi Agosti, zaidi ya wapiga kura milioni 22, watashiri zoezi la kuwachagua viongozi wao, huku tetesi zikiibuliwa iwapo sajili ya chapa na ile ya kielektroniki zitakuwa katika vituo vya kupiga kura.

Licha ya kuwa tume ya Uchaguzi na Uratibu wa mipaka hapa nchini IEBC imedinda kutumia sajili ya chapa, baadhi ya mirengo ya kisiasa inaendelea kushinikiza kuwepo kwa sajili hiyo.

Hata hivyo la muhimu zaidi wakati wa zoezi la upigaji kura, ni kufahamu mchakato mzima wa upigaji kura, pamoja na haki alizonazo mpiga kura.  Umuhimu mkubwa wa kufahamu taratibu za upigaji kura kwanza ni kuhakikisha kuwa kura haziharibiki wala mpiga kura hakosi nafasi ya kumchagua kiongozi anayempenda.

Katika Uchaguzi Mkuu ujao, wapiga kura watawachagua viongozi sita. Wao ni pamoja na Rais na naibu wake, Gavana na naibu wake, Mwakilishi mwanamke, Seneta, Mbunge wa bunge la taifa na Mwanachama wa bunge la kaunti.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.

Shirika la utangazaji nchini KBC kwa ushirikiano na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, iliandaa zoezi la muigo la upigaji kura, kwa lengo la kuhakikisha wakenya wanafahamu vyema taratibu za kupiga kura.

Utaratibu wa kupiga kura

Afisa wa tume ya IEBC Amina Suud, alielezea hatua moja baada ya nyingine mchakato mzima wa upigaji kura. Kulingana na Amina kwanza kabisa mpiga kura anapaswa kuwasili kwa kituo  alichosajiliwa kupiga kura. Mpiga kura huyo ataandamana na stakabadhi alizotumia kujisajili, iwe ni kitambulisho cha taifa au ni pasipoti ya kusafiri.

Also Read
Sossio ashtumiwa kwa kutotetea vilivyo chama cha KNUT

Aidha kulingana na Amina iwapo mpiga kura alijisajili kutumia Pasipoti, na tayari imepitwa na wakati, basi atahitajika kuwasilisha Pasipoti hiyo ya awali na Pasipoti mpya.

“Ikiwa alisajiliwa na Pasipoti na imepitwa na wakati, itabidi aje na hiyo aliyotumia kusajiliwa na mpya iliyotengenezwa”alisema Amina Suud, afisa wa IEBC.

Hatua ya pili baada ya mpiga kura kuwasili katika kituo cha kupiga kura, ni stakabadhi zake kukaguliwa kuhakikisha ni halali. Kisha afisa wa IEBC atakagua vidole vyake kuhakikisha haina rangi kuthibitisha hajapiga kura.  Iwapo itabainika hajapiga kura, basi ataruhusiwa kuweka kidole kwenye mtambo wa kuwatambua wapiga kura.

Wakenya washiriki zoezi la upigaji kura. Hisani

Kulingana na Amina, afisa wa tume ya IEBC, iwapo mpiga kura hatapatikana kupitia kuweka kidole katika mtambo, basi hatua ya pili hutumiwa ambayo ni Alphanumeric, mfumo ambao hutumia nambari za kitambulisho cha taifa au zile za Pasipoti. Iwapo bado hatapatikana kupitia mfumo huo wa Alphanumeric, basi itabainika kuwa mtu huyo si mpiga kura katika kituo hicho na ataelekezwa vilivyo.

Na mtu huyo akithibitishwa kuwa yeye ni mpiga kura katika kituo hicho, basi ataelekezwa katika hatua inayofuata ambapo sasa atakabidhiwa karatasi za kupiga kura ambazo ni sita.

“Mpiga kura atakutana na karani wa kwanza ambaye atamkabidhi karatasi mbili za kupiga kura, karani wa pili na wa tatu pia watamkabidhi karatai mbili kila mmoja za kupiga kura,”alieleza Amina Suud afisa wa tume ya IEBC.

Katika kituo cha kupiga kura, kuna sehemu ambayo imetengwa faraghani ambapo mpiga kura atatumia kuweka alama katika karatasi za kupiga kura, kumchagua kiongozi wake. Akishamaliza kufanya hivyo atatumbukiza karatasi hizo ndani ya sanduku.

Also Read
Kituo cha malipo cha barabara ya Expressway Mlolongo chafungwa

La muhimu kwa mpiga kura ni kwamba kila sanduku lina kifuniko ambacho kina rangi sawia na karatasi ya kupiga kura. Mpiga kura anapaswa kuweka kila karatasi ndani ya sanduku lililo na rangi sawia na karatasi. Baadaye mpiga kura atawekwa alama katika kidole na kuruhusiwa kuondoka katika kituo cha kupiga kura.

Tume huru ya Uchaguzi na mipaka IEBC imeweka mipango maalum kwa wapiga kura  walio na mahitaji mbali mbali. Kulingana na Amina Suud, mpiga kura aliye na mahitaji maalum, ataruhusiwa kuwa na msaidizi wake. Msaidizi huyo pia atawekwa rangi katika kidole kuthibitisha kuwa hatatoa usaidizi kwa mtu mwingine.

Msaidizi huyo atahitajika kuchukua kiapo cha siri, kuhakikisha hatoi siri ya aliyemsaidia kupiga kura.

Aidha ni muhimu kwa mpiga kura kuhakikisha kila karatasi ya kupiga kura inawekwa muhuri wa tume ya IEBC. Ikiwa muhuri itasahaulika, basi “Kura hiyo hatutaihesabu na itakuwa kura ambayo imeharibika,” alisema Amina Suud afisa wa tume ya IEBC.

Kuharibika kwa Kura

Swali ambalo huwakuna wengi vichwa ni je, Kura iliyoharibika ni ipi? Kulingana na tume ya IEBC, kura ambayo imeharibika ni ile iliyo na alama zaidi ya Moja katika karatasi moja ya kupiga kura au ni ile iliyo na alama isiyofaa kama vile kuchora umbo fulani au kuweka sahihi.

Also Read
Rais Kenyatta amwomboleza mzee Edward Kiprotich Karoney

“Usiweke alama ambayo haifaii katika karatasi ya kupiga kura, wala usichore chochote katika karatasi ya kupiga kura, na pia usiweke alama zaidi ya moja,”alifafanua Amina Suud afisa wa IEBC.

Kura ambazo zimeharibika hazitahesabiwa.

Mavazi siku ya Kupiga kura

Ili kuhakikisha sheria za uchaguzi zinadumishwa, wapiga kura hawataruhusiwa kuvalia mavazi ya kampein, ambayo yanajumuisha kofia, shati au shuka zinazompigia debe mwaniaji fulani wa kisiasa.

“Ni hatia kwa mpiga kura kuvalia mavazi ya kampein wakati wa siku ya kupiga kura. Ikifika saa 48 kabla ya siku ya kupiga kura, ni vyema uoshe hayo mavazi yako na uyaweke, bila hivyo utachukuliwa hatua,”alisema Amina.

Zoezi la IEBC la kuhesabu kura.

Kuhesabiwa Kura

Kinyume na hapo awali ambapo kura zilihesabiwa katika kituo cha kujumlisha kura, tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, imesema kuwa kura zitahesabiwa katika kituo cha kupiga kura, ili kuondolea mbali tashwishi zozote.

Kulingana na Mwenyekiti wa tume ya huru ya Uchaguzi na mipaka IEBC, mawakala wa vyama vya kisiasa na pia wanahabari wataruhusiwa kupiga picha nakala ya matokeo ya uchaguzi katika kituo cha kupiga kura.

“Kupiga picha nakala hiyo kutawasaidia wawaniaji kuweza kulinganisha matokeo yanayotangazwa katika makao makuu na matokeo yaliyonakiliwa katika kituo cha kupiga kura,” alisema Wafula Chebukati mwenyekiti wa tume ya IEBC.

Wafungwa watapiga Kura

Tume ya IEBC imethibitisha kuwa wafungwa wataruhusiwa kupiga kura, lakini watapiga kura Urais peke yake. Aidha mikakati kabambe imewekwa kuhakikisha zoezi hilo katika magereza ya humu nchini linakuwa shwari bila dosari.

  

Latest posts

Maendeleo ya Wanawake yampongeza Rais kwa kuwateuwa wanawake mawaziri

Dismas Otuke

NMS yakabidhi majukumu yake kwa kaunti ya Nairobi

Tom Mathinji

KBC Channel One na Idhaa 13 kupeperusha mechi za kipute cha kombe la dunia

Dismas Otuke

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi