Jenerali Kibochi: Jeshi lina jukumu la kuisaida serikali katika nyanja zote

Nidhamu, maadili mema, kujitolea na utaalamu ni nguzo nne kuu muhimu ambazo hutoa mwongozo katika oparesheni za vikosi vya ulinzi vya kenya, KDF. Haya ni kwa mujibu wa mkuu wa vikosi vya ulinzi Jenerali Robert Kibochi.

Matokeo ya nguzo hizo nne  ni ya kuridhisha na hata kusababisha Rais Uhuru Kenyatta kujukumu vikosi vya KDF kufufua baadhi ya taasisi za serikali zilizokuwa zimesitisha utoaji huduma na ambazo hazikuwa na usimamizi bora.

Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Kenya Jenerali Robert Kariuki Kibochi akizungumza na runinga ya KBC Channel1, alisema nidhamu husaidia pakubwa kuondoa maslahi ya kibinafsi.

KDF huhakikisha nidhamu inadumishwa kuanzia siku ya kuanza mazoezi kwa makurutu. Hilo ndilo swala ambalo hutenganisha KDF na taasisi zingine,” alisema Kibochi.

Mkuu huyo wa vikosi vya KDF alisema kuwa mtu mwenye maadili mema huweza kuaminika na wafanyikazi wenzake, akiongeza kuwa hali ya kutokuwa na ubinafsi ni kujitolea kuhakikisha ufanisi.

Hata hivyo, Jenerali huyo alitaja utaalamu kuwa jambo la muhimu sana. Alidokeza kuwa mazoezi na elimu, huboresha utaalamu katika vikosi vya ulinzi hapa nchini.

Kibochi alisema usalama na maendeleo ya nchi huenda sambamba na kwamba jeshi la nchi lina jukumu la kuisaidia katika nyanja ambazo serikali itahitaj usaidizi.

Ukarabati wa reli ya kutoka Nairobi kuelekea Nanyuki, ni mojawepo wa majukumu tunayotekeleza. Tuna utaalamu katika nyanja zote, Uhandisi na utabibu zikiwemo, mbona tusizitumie kusaidia nchi yetu?,” aliuliza Kibochi.

Kulikuwa na manung’uniko wakati Rais Uhuru Kenyatta alipohamisha tume ya utayarishaji na uuzaji nyama nchini KMC kwa wizara ya ulinzi mwezi Septemba mwaka 2020. Jenerali kibochi alisema kituo cha KMC cha Athi River hakikuwa kikifanya kazi, kwani kilikosa vifaa vya kisasa na usimamizi wake ulikuwa mbovu.

Tuliwaleta wataalam kutoka kitengo cha teknojia ya habari, na pia kuwahusisha madaktari wa mifugo na kwa muda mfupi sana kituo hicho kikaaza kufanya kazi ipasavyo. Ukizungumza na wafugaji wanaouza mifugo wao kwa KMC, watakuelezea furaha yao. Wanapowasilisha mifugo, wao hulipwa katika muda wa saa 72,” alisema mkuu huyo wa jeshi la kenya.

Hata hivyo Kibochi alisema vikosi vya ulinzi vinakusudia kuanzisha kampuni ya ujenzi ili kutekeleza shughuli za ujenzi katika maeneo yaliyo na changamoto za kiusalama humu nchini,huku kikitoa ulinzi katika maeneo hayo.

Kuna baadhi ya sehemu ambapo wanakandarasi hawawezi tekeleza miradi kutokana na ukosefu wa usalama, na tunahitajika kuwapatia ulinzi. Si itakuwa vyema ikiwa vikosi vya ulinzi vitakuwa na kampuni ya ujenzi? Wanajeshi hawatahitaji ulinzi wanapofanya kazi hiyo na itapunguzia serikali gharama,” aliongeza Kibochi.

Kibochi alidokeza kuwa wahandisi wa kikosi cha jeshi la wanamaji walitumia shilingi milioni 50 kukarabati MV Uhuru licha ya kuwa wanakandarasi wa kibinafsi walikuwa wameitisha shilingi bilioni 1.5.

Tuko tayari kutekeleza jukumu lolote ambalo tutapatiwa na amiri jeshi mkuu. Tuna uwezo ikizingatiwa kwa sasa tuna madaktari wanaofanya kazi na wizara ya Afya tangu kuzuka kwa virusi vya Covid-19 hapa nchini mwezi Machi mwaka 2020. Hakuna makosa yoyote kwa kuhusisha jeshi. Vikosi vya ulinzi ni rasilimali muhimu kwa serikali,”alisema Kibochi.

Jenerali Kibochi aliteuliwa kuwa mkuu wa vikosi vya ulinzi hapa nchini tarehe nne mwezi Mei mwaka 2020, baada ya kujiunga na jeshi la Kenya mwaka 1979.

Jenerali huyo ameshikilia nyadhifa mbali mbali katika vikosi vya ulinzi ambazo ni pamoja na naibu mkuu wa vikosi vya ulinzi nchini, kamanda wa vikosi vya nchi kavu na kamanda wa kikosi cha kenya katika umoja wa mataifa nchini Sierra Leone miongoni mwa zingine.

  

Latest posts

Shule za umma zina uwezo wa kuandikisha matokeo bora iwapo zitajikakamua zaidi

Tom Mathinji

Mzozo wa kidiplomasia kati ya Uchina na nchi za magharibi wasitishwa

Tom Mathinji

Musalia Mudavadi apuuzilia mbali dhana ya ma-‘Hustler’

Tom Mathinji

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi