Kenya na Tanzania zajitolea kuboresha uhusiano baina yazo

Rais wa Tanzania anayezuru humu nchini,Samia Suluhu Hassan,alikutana na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Nairobi Jumanne, ambapo walijadiliana kuhusu Biashara,ushirikiano wa kanda hii na masuala ya usalama.

Akiongea na wanahabari baada ya mkutano huo wa masaa mawili, Rais Uhuru Kenyatta alimpongeza Rais Suluhu kwa kuchaguliwa hivi majuzi kuwa mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi CCM.

Also Read
Vyuo vikuu vyatakiwa kuwekeza katika mtaala mpya wa CBC

Rais Kenyatta alisema kenya itafanya kazi kwa pamoja na Tanzania, kwa lengo la kuimarisha uchumi kwa manufaa ya watu wa nchi hizi mbili za Afrika Mashariki.

Alisema tume ya pamoja ya ushirikiano na mawaziri kutoka nchi hizi mbili watakuwa wakikutana mara kwa mara, ili kusuluhisha masuala yanayotatiza uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Tanzania.

Aidha kiongozi wa taifa aliongeza kwamba ipo haja ya kuimarisha biashara, reli na uchukuzi wa angani kati ya nchi hizi mbili ili kurahisisha kufanya biashara.

Kwa upande wake, Rais Suluhu Hassan wa Tanzania, alisema Kenya imeorodheshwa mshirika wa kwanza wa biashara wa Tanzania na wa tano duniani huku akidokeza kuwa Tanzania itaimarisha zaidi uwekezaji wake wa kibiashara nchini Kenya.

Suluhu alisema mawaziri kutoka nchi hizi mbili watakuwa wakikutana mara kwa mara ili kushughulikia changamoto zinazotokana na janga la COVID 19 kwa lengo la kuhakikisha biashara na utangamano kati ya nchi hizi mbili hazitatizwi.

Rais Suluhu anatarajiwa kuhutubia kikao cha pamoja cha mabunge yote mawili siku ya Jumatano.

  

Latest posts

Mwanafunzi ateketeza bweni kukwepa kufanya mitihani Tharaka Nithi

Tom Mathinji

Mahakama yamzuia Mohammed Badi kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri

Tom Mathinji

IEBC yalenga kuwasajili wapiga kura wapya milioni sita kabla Uchaguzi Mkuu ujao

Tom Mathinji

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi