Vita dhidi ya ugonjwa wa macho aina ya Trachoma ambao husababisha upofu, vimepigwa jeki baada ya Kenya na Uganda kuzindua shughuli za pamoja za kutibu ugonjwa huo kwa raia wanaoishi katika mpaka wa nchi hizi mbili.
Shughili hiyo ya kutoa dawa inayotekelezwa na Kenya na Uganda inanuiwa kuwianisha utoaji dawa miongoni mwa wakazi wa kaunti za Pokot-magharibi na Turkana na wakazi wenzao kutoka nchi jirani ya Uganda.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa shughuli hiyo katika shule ya msingi ya Alakas katika wilaya ya Amudat nchini Uganda, Waziri wa Uganda anayehusika na masuala ya jamii ya Karamoja, Dkt. Maria Goretti alieleza kuridhishwa na mpango huu wa hivi punde akisema utahakikisha jamii zinaoishi kwenye mpaka wa pamoja wa Kenya na Uganda zinapokea matibabu haya yanayohitajika mno.
Goretti alisema wakati wa juhudi za awali za serikali za nchi hizi mbili ambapo ziliandaa mipango ya kutoa dawa kwa umma nyakati tofauti, jamii za sehemu hiyo ziliachwa nje kutokana na mitindo yao ya maisha ya wafugaji wa kuhama hama.
Akizungumza katika hafla hiyo, mkuu wa idara ya maradhi ya kuambukizwa na yale yaliopuuzwa katika maeneo yenye joto katika wizara ya afya, Wycliffe Omondi, alisema ipo haja ya kuwepo juhudi za pamoja katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa eneo hili linatarajiwa kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa macho wa Trachoma.
Mpango wa kitaifa wa kukabiliana na ugonjwa wa Trachoma wa mwaka 2021, unalenga kuwatibu watu 2,826,638 katika kaunti saba ambazo ni Baringo,Isiolo, Kajiado, Narok, Samburu, Turkana na Pokot Magharibi.