Kenya imeanza kutoa chanjo ya pili ya dawa ya Oxford-AstraZeneca baada ya kutamatisha awamu ya kwanza ya mpango huo wa chanjo.
Siku ya Ijumaa waziri wa afya Mutahi Kagwe alisema wale wote waliotarajia kupata chanjo ya pili wanaendelea kujulishwa kupitia kwa ujumbe mfupi, na kuwashauriwa wafike kwenye vituo vyao vya chanjo.
Alisema kwa mara nyingine nafasi ya kwanza itatolewa kwa wahudumu wa afya, ambao walipewa chanjo ya kwanza mwanzoni mwa kampeini hiyo mwezi Marchi.
Utoaji huo wa chanjo ya pili unajiri wiki 12 baada ya kutolewa chanjo ya kwanza kuambatana na maagizo ya shirika la afya duniani (WHO).
Siku ya Jumamosi Kenya itapokea dozi elfu-72 za dawa ya AstraZeneca kutoka Sudan Kusini na pia Jamhuri ya Ki-demokrasia ya Congo, kama ilivyotangazwa awali.
Kulikuwa na hali ya wasiwasi kutokana na usambazaji wa chanjo hiyo baada ya India kusitisha usambazaji wake kutokana na Idadi kubwa ya visa vya Covid-19 vinavyoghubika taifa hilo.