Mipango yote imekamilika kupokea kombe la kifahari la dunia likitarajiwa kuwasilishwa nchini Mei 26 .
Ziara ya kombe ilianza wiki jana mjini Dubai na inatarajiwa kuzungushwa katika mataifa 22 kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu.
Katika ziara hiyo mashabiki nchini Kenya watapata firsa ya kulitazama na kupiga nalo picha kati ya Mei 26 na 27 ,punde baada ya hafka hiyo kuandaliwa nchini Ethiopia baina ya tarehe 24 .
Baada ya msafara wa Kenya Kombe hilo litaelekea nchini afrika Kusini ambapo mashabiki watalitazama kati ya tarehe 28 na 30 ,na kisha kurejea kupelekwa Tanzania baina ya Mei 31 na Juni Mosi.
Kombe hilo litapokelewa na maafisa wakuu serikali tarehe 26 mwezi huu na kupelekwa katika Ikulu ya Rais , kabla ya uma kulitazama katika ukumbi wa mikutano ya kimataifa KICC Mei 27.
Kampuni ya Cocola inaongoza hafla hiyo ambapo kombe hilo litazungushwa katika mataifa 51 yakiwemo 22 katika awamu ya kwanza kati ya Mei na Juni ,na mengine katika awamu ya pili kati ya Agosti na Novemba mwaka huu ikiwemo katika mataifa yote 32 yaliyofuzu kwa fainali za kombe dunia mwaka huu .
Kombe la dunia la sasa ni la uzani wa kilo 6 nukta 142 na limeundwa kwa dhahabu na desturi huwa ni wachezaji wanaotawazwa mabingwa au waliowahi kuwa mabingwa wa dunia pamoja na Marais wa mataifa linapozungushwa ambao huruhusiwa kulibeba.
Makala ya 22 ya kindumbwendumbwe cha kombe la dunia yataandaliwa kati ya Novemba 21 na Disemba 18 mwaka huu nchini Qatar yakiwa mashindano ya mwisho kushirikisha mataifa 32.