Huku taifa hili likiandaa mikutano ya kimataifa, bodi ya utalii humu nchini (KTB), imetoa wito kwa wahudumu wa sekta ya utalii na wadau wengine wa sekta hiyo, kuchukua fursa ya makongamano na mikutano ya kibishara inayoandaliwa humu nchini kutangaza shughuli za kitalii humu nchini.
Afisa mkuu mtendaji wa bodi hiyo Dk. Betty Radier, amesema baada ya kuwa mwenyeji wa hafla hizo, Kenya imethibitisha uwezo wake wa kuwa mwenyeji wa makongamano ya ngazi za juu ya kimataifa.
“Kama taifa tumethibitisha uwezo wetu wa kuandaa mikutano ya kimataifa ya hadhi za juu. Hii inatupatia fursa ya kuwa na wageni wengi na hivyo kuwavutia katika utalii wa humu nchini,” alisema Radier.
Dkt. Radier ametoa wito kwa wahudumu wa sekta hiyo kuunaganisha shughuli za kibiashara na kitalii akisema Kenya imetimiza masharti yanayohitajika kwa shughuli za kitalii.
Kwa upande wake afisa mkuu mtendaji wa chama cha utalii cha Ziwa Victoria Charles Kataro amesema uunganishaji wa biashara na utalii unafanyika kote duniani.
Ametoa wito kwa serikali na wadau wengine kuendelea kushinikiza hafla muhimu kuandaliwa humu nchini ili kuongeza idadi ya watalii wanaozuru taifa hili.