Madonna azuru Kenya

Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Marekani Madonna alizuru Kenya na siku ya Jumamosi, alipachika video kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa na watu wa eneo la Samburu.

Madonna ambaye pia ni muigizaji, alionekana akifurahia utamaduni wa watu wa eneo la Samburu huku akielezea kwamba ni wafugaji wa kuhama hama na kusifia densi yao na hadithi zao.

Madonna alizuru pia eneo la Pokot na watu wa eneo hilo wanaonekana kufurahia ujio wake huku wakimchezea densi ya kitamaduni.

Alikuja Kenya baada ya kuzuru nchi ya Malawi ambako alifungua shule ya kucheza densi baada ya kuzuru shule ya mayatima ya Jacaranda.

Alikaa nchini Malawi kwa muda wa wiki moja ambapo alitekeleza mambo kadhaa ya kusaidia jamii kupitia kwa shirika lake kwa jina “Raising Malawi”.

Shule hiyo ya densi jijini Blantyre nchini Malawi inaitwa “Madame x dance Studio” inalenga kusaidia watoto wa Jacaranda na itaendeshwa na shirika lake la usaidizi nchini Malawi.

Madonna alisifia sana shule ya Jacaranda akisema waanzilishi na waalimu hujitolea kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu na kwamba wanafunzi wana talanta mbali mbali ambazo ni njia mwafaka ya kujieleza.

Alizungumzia mwaka 2020 ambao ulikuwa mgumu kutokana na janga la Corona lakini kulingana naye mambo ni magumu zaidi nchini Malawi.

Alisema densi ndiyo anapenda zaidi huku akihimiza kila mmoja katika jamii ya Jacaranda ajiamini na kuamini katika ndoto zake.

Katika ziara yake ya mwaka huu, Madonna aliandamana na watoto wanne ambao aliasili na anaishi nao na kuwatunza nchini Marekani.

Amewahi kujihusisha pia na mipango kadhaa ya usaidizi nchini Kenya na hata mpango wa afya wa “Beyond Zero” unaoendeshwa na mama taifa Bi. Margaret Kenyatta.

  

Latest posts

Rayvanny Kumtambulisha Msanii wa Kwanza NLM

Marion Bosire

Dulla Makabila Ajiondolea Lawama

Marion Bosire

Mwigizaji Atoa Ilani Kwa Rais Museveni

Marion Bosire

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi