Wamiliki wa magari wamepata afueni ya muda baada ya mahakama kuu kusimamisha utekelezaji wa nyongeza ya malipo ya bima ya magari ambayo ilianza kutekelezwa mwezi huu.
Jaji James Makau pia alisimamisha utekelezaji wa uamuzi wa kampuni za bima wa kukosa kutoa bima ya fidia kamilifu yaani comprehensive insurance kwa magari ambayo yalitengenezwa zaidi ya miaka 12 iliyopita au yale ambayo thamani yake ni chini ya shilingi laki sita hadi kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa.
Jaji Makau alisema kusimamishwa kwa hatua hiyo ni muhimu kwa vile kesi iliyowasilishwa na tume ya kutetea haki za binadamu inaweza kufaulu hasaa kwa kuzingatia maswala yaliyoibuliwa katika kesi hiyo.
Kampuni za bima zilisema kuwa kuongezwa kwa malipo hayo kunalenga kufidia hasara ambayo zimekuwa zikipata katika miaka iliyopita katika kiwango hicho cha bima ya comprehensive insurance.
Kampuni hizo zinadai kuwa kiwango cha pesa zinazodaiwa kama fidia, kimezidi kiwango cha pesa ambazo zinakusanywa kutokana na kuongezeka kwa ajali za barabarani.